December 7, 2015

Magufuli Ateka Kampeni za Urais Uganda kwa Museveni......Wapinzani Watumia Jina Lake Kuomba Kura


Kasi ya Rais John Magufuli katika kubana matumizi yasiyo ya lazima ya serikali ili fedha zinazookolewa zielekezwe katika kuimarisha huduma za jamii imeendelea kuvutia wengi katika nchi jirani za Afrika Mashariki baada ya jina lake kuanza kutumiwa na wagombea urais nchini Uganda.

Kati ya wagombea wote, aliyejipambanua kwa uwazi kuwa atafuata nyayo za Magufuli katika kuhakikisha kuwa serikali inaendesha mambo yake kwa nia ya kubana matumizi yasiyo ya lazima, kukomesha ufisadia na mwishowe kuwanufaisha watu wa tabaka la chini kupitia uboreshaji wa huduma za jamii ni mgombea wa upinzani anayemtikisa Rais Yoweri Museveni katika kinyang’anyiro hicho, Dk. Kizza Besigye wa chama cha Forum for Democratic Change (FDC). 

Katika kampeni zake mwishoni mwa wiki, Besigye amesema wazi kuwa pindi atakapochaguliwa na wananchi na kuingia madarakani, atafuata nyayo za Magufuli kwa kuanza kuipiga bei ndege  inayotumiwa na Museveni kwa maelezo kuwa inalibebesha taifa lao gharama kubwa ambazo zinaweza kutumiwa katika kuboresha huduma za jamii.

Uchaguzi Mkuu nchini Uganda unatarajiwa kufanyika mwanzoni mwa Februari, 2016.

Akiwa amefuatana na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Profesa Ogenga Latigo, kwenye mkutano wa kampeni wilayani Agago nchini humo, Besigye ambaye pia ni Kanali wa Kijeshi, alisema ataiuza ndege hiyo aina ya  Gulfstream V Jet, iliyoligharimu taifa hilo shilingi za Uganda bilioni 88.2 (Sh. bilioni 55.6 za Tanzania).

Besigye alisema ndege hiyo haiongezi faida yoyote kwa walipa kodi wa Uganda, licha ya Rais Museveni kudai kuwa anaitumia tu wakati akitaka kusafiri nje ya nchi, hoja ambayo Besigye anaipinga kwa kuwa hata kama haitumii kwa safari za ndani, bado inatakiwa mashine zake zitunzwe na wafanyakazi wake pia wahudumiwe.

Besigye alisema yeye anaunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais mpya wa Tanzania, Magufuli, ambaye anaishi kulingana na jina lake la utani la ‘tingatinga’ kutokana na kuchukua hatua kadhaa dhidi ya ufisadi, kuongeza ufanisi wa kazi katika ofisi za umma na pia kuongeza nidhamu ya matumizi kwa manufaa ya taifa na siyo watu wachache.

Magufuli amekuwa akiwavutia Watanzania wengi wa kawaida huku akijielekeza katika kuhakikisha kuwa anashughulikia kero za wananchi ambazo zimekuwa zikisababishwa na tabaka la watawala na wafanyabiashara ambao wamekuwa wakijitajirisha wenyewe. 
 
Besigye anaonekana kumuiga Magufuli kwa kuelekeza kampeni zake katika kushughulikia kero za wananchi wa kawaida.

Aidha, katika kufuata zaidi nyayo za Magufuli, Besigye amekuwa akizungumzia masuala yanayohusu hatma ya kila siku ya maisha ya watu wa kawaida, hasa kina mama wasioweza kupata fedha zinazotozwa kwao wakati wa kujifungua. 
 
Kadhalika, Besigye amekuwa akizungumzia vijana wanaohaha kutafuta kazi kila uchao baada ya kumaliza shule na pia wananchi wengine ambao wengi wanakabiliwa na lindi kubwa la umaskini.

No comments:

Post a Comment