January 28, 2015

Diamond, Ali Kiba Uchawi Watawala, Hirizi zaokotwa Uwanjani Moja Yakutwa Ikipumua



HALI inazidi kuwa mbaya kwa mastaa wawili wa muziki wa Bongo Fleva wanaogombea unyota kimuziki, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Ali Saleh Kiba, safari hii yameibuka mapya kwa kila msanii kuogopa kumshika mkono mwenzake kutokana na imani za kishirikina.

TUJIUNGE LEADERS
Matukio hayo ya kusisimua yaliwatia hofu kubwa mashabiki na wadau wa muziki Bongo muda mfupi kabla ya nyota hao kukaribishwa stejini kwenye Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar, mwishoni mwa wiki iliyopita.

HIRIZI ZAKUTWA UWANJANI
Kwa mujibu wa wanahabari wetu, katika Viwanja vya Leaders, Kinondoni, kulikutwa hirizi zilizozagaa, zilizodaiwa kudondoshwa  na vijana waliokamatwa wakiwa wamevalia sare zenye majina ya mastaa hao wawili.


Katika hali ya kushangaza, mmoja wa mashabiki waliohudhuria onyesho hilo ambaye aliziona hirizi hizo, aliwashangaza mashabiki wenzake alipodai kuwa anaiona mojawapo ikitweta mithili ya inayopumua!
“Oneni wadau, hii hirizi si inapumua, iangalieni vizuri,” alisikika shabiki huyo na kuwaacha watu wakiwa wamepigwa na butwaa kuona vitendo hivyo vya kishirikina katika eneo la burudani.


Wakati matukio hayo ya kukutwa kwa hirizi hizo yakiendelea, Diamond, baada ya kupanda jukwaani kabla ya kuanza kuimba, akajikuta akiteleza na kuanguka jukwaani na kusimama mwenyewe huku vijana wanaodaiwa kuwa ni wa Timu Kiba wakipiga kelele kwa nguvu kuashiria kuwa walipendezewa na kitendo hicho kutokea.

Pamoja na Diamond kula mwereka hadi chini, hali ilizidi kuwa mbaya kwake baada ya muziki kuanza kusikika vibaya huku ukiwa unakatakata, kitendo kilichoamsha hisia kuwa kulikuwa na ushirikina unaoendelea ili kumshusha kisanii kwa kuonekana amefanya vibaya katika shoo hiyo

CHUPA ZARUSHWA
Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya huku chupa za maji zikirushwa jukwaani hapo na baadhi zikimpiga na nyingine akizikwepa wakati akiendelea kupiga shoo, Diamond aliamua kutumia akili ili kuzima kelele hizo kwa kuanza kumwaga noti.

Ishu hiyo iliwafanya mashabiki na Timu Kiba kuachana na zoezi hilo na kuanza kusukumana kugombea noti hizo za elfu mbilimbili ambapo alimwaga kwa awamu tatu.

SADAKA?
Wakati akizidi kuwatupia noti mashabiki, Diamond alisikika akisema kuwa pesa hizo ni maalum kwa mashabiki kwani ni sadaka kwao kutokana na sapoti kubwa wanayompa ingawa hataweza kumpa kila mmoja.

DIAMOND KAMA MICHAEL JACKSON
Hata hivyo, baadhi ya mashabiki waliokuwa wakisukumana na kuokota noti hizo walisikika wakisema:
“Huu mchezo alikuwa akiufanya Michael Jackson (Mwanamuziki marehemu wa Marekani) tena alikuwa akitumia ushirikina na Freemasons.
“Michael alikuwa anadaiwa kumwaga fedha hizo zilizokuwa na nguvu ili kuwafanya wale waliokuwa wakimzomea kukaa kimya,” alisikika shabiki mmoja akisema.

MSHANGAO
Katika hali ya kushangaza zaidi,  Diamond alivua tisheti na vesti ya ndani na kujifuta jasho kisha kuwarushia mashabiki huku akijua wazi kuwa amefutia jasho lililokuwa likimiminika mwilini mwake kama maji.


KIBA HAKUTAKIWA KUZUNGUMZA?
Wakati matukio ya kushangaza aliyokuwa akiyafanya Diamond na yale ya kurushiwa chupa za maji machafu na yenye mikojo yakiendelea, ilidaiwa kuwa Kiba alipoingia kwenye chumba cha wasanii hakutaka kuzungumza na mtu yeyote huku ikidaiwa kuwa hiyo ni ishara kubwa kuwa hakutakiwa kuzungumza na mtu kwani angeweza kupoteza nguvu za kufanya shoo.

POLISI MZIGONI
Wakati mashabiki wakizidi kuwa na wasiwasi juu ya wasanii hao, jeshi la polisi lililokuwa na zana zote za kukamatia wahalifu, walianza doria ya kukamata vijana ambao wanadaiwa kuwa ni Timu Kiba waliokuwa wakibishana na kutupa chupa zenye mikojo na maji  huku wakipokea kipigo kama cha mbwa mwizi.

KIBA ARUKA UKUTA
Awali kabla ya shoo hizo kuanza matukio ya kishirikina yalijidhihirisha zaidi baada ya Ali Kiba kuingia uwanjani hapo kwa njia ya kuruka ukuta na hata alipozama kwenye chumba maalum walichokuwa wametengewa wasanii hakuweza kushikana mikono na wenzake.Wasanii ambao Ali Kiba aliwachunia ni AY, MwanaFA, Shaa, Shilole, Vanessa Mdee na Jux, ambao wote aliwakuta ndani ya chumba hicho.

Credit Globalpublisher

No comments:

Post a Comment