KESI
za kupinga matokeo ya ubunge zimezidi kumiminika katika Mahakama Kuu ya
Tanzania Kanda ya Mwanza, ikiwamo za kupinga matokeo yaliyompa ushindi
Mbunge wa Bunda Mjini Ester Bulaya (Chadema).
Kesi
nyingine zilizofunguliwa mahakamani ni za majimbo ya Nyamagana, Ilemela
na jimbo la Kwimba, ambapo walalamikaji wamewasilisha malalamiko mbali
mbali ikiwamo ya vitendo vya rushwa.
Kesi
ya kwanza iliyofunguliwa ni ya ubunge wa Jimbo la Bunda Mjini ambayo
imefunguliwa na Magambo Masato na wenzake watatu wakipinga matokeo
yaliyompa ushindi Mbunge wa Jimbo hilo, Ester Bulaya.
Kesi
hiyo namba 1 ya mwaka 2015 mara ya kwanza ilifunguliwa Novemba 18 mwaka
huu, juzi ilikuwa mara ya kwanza kupelekwa mahakamani kwa ajili ya
kutajwa.
Kesi
hiyo ambayo ipo kwa Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya
Mwanza, Francis Kabwe, walalamikaji wa kesi hiyo wamewasilisha
malalamiko mahakamani hapo wakidai kwamba Bulaya alipata ushindi kwa
njia ya rushwa.
Bulaya aweka pingamizi
Mlalamikiwa
katika kesi hiyo, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Ester
Bulaya, mapema juzi aliwasilisha hoja za msingi kuweka pingamizi kwa
walalamikaji kufungua kesi mahakamani.
Hoja
alizowasilisha Bulaya ni kwamba walalamikaji hawana mamlaka ya kufungua
na kuendesha kesi ya aina hiyo kwani hawajaonesha ni namna gani
imeathiri haki zao kama wapiga kura.
Pili
katika shauli walillowasilisha mahakamani hawakuonesha ni namna gani
vitendo vya rushwa walivyodai vilikuwa vikifanywa na Mawakala wa Bulaya
havijaoneshwa, pia shauri hilo limekiuka kifungu cha 12 (D) cha sheria
ya uchaguzi.
Hata hivyo kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 29 mwaka huu, itakapo tajwa tena mahakamani hapo kwa ajili ya kuisikiliza.
Kesi ya Wenje
Aliyekuwa
Mgombea ubunge Jimbo la Nyamagana mkoani Mwanza, Ezekiah Wenje, juzi
alitinga Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, kuomba kupunguziwa
gharama za uendeshwaji wa kesi.
Pia
Wenje katika kesi hiyo anawashitaki, Mbunge wa Nyamagana Stanslaus
Mabula (CCM), Msimamizi wa Uchaguzi huo, Tito Mahinya na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali.
Hata
hivyo amewasilisha malalamiko mahakamani hapo kwamba uchaguzi huo
haukuwa haki na huru, kwenye uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Hata
hivyo katika kesi hiyo namba 3 ya mwaka 2015, Wenje aliwakilishwa
mahakamani hapo na Wakili Outa na upande wa walalamikiwa waliwakilishwa
na Wanasheria wa Serikali, Mtalemwa, Kitia Tuloke na Ajuaye Bilishaga.
Kesi ya Highness Kiwia
Novemba
25 mwaka huu aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Ilemela, Highness Kiwia,
alifungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza ya kupinga
matokeo yaliyompa ushindi, Angelina Mabula (CCM) pamoja na kuwashitaki
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi huo, John Wanga.
Kesi
hiyo namba 2 ya mwaka 2015, mlalamikaji katika kesi Kiwia hakufika
mahakamani hapo, ambapo kwa upande wa walalamikiwa waliwakilishwa na
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Malongo.
Kesi
ya Wenje na Kiwia zimeahirishwa ampapo ya Wenje itatajwa Desemba 10
mwaka huu na ya Kiwia hadi Desemba 14 mwaka huu, huku Msajili, Kabwe
amedai kuwa endapo siku hiyo mlalamikaji Kiwia hatatokea kesi
itatupiliwa mbali.
No comments:
Post a Comment