\
Namshukuru Mwenyezi Mungu aliyeiwezesha nchi yetu kutimiza miaka 54 ya uhuru kwa salama na amani.
Namshukuru Mungu pia kwa kuniwezesha kuiona siku hii nikiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Napenda kuchukua fursa hii, kuwapongeza Watanzania wenzangu kwa Taifa letu kutimiza 54 ya Uhuru tarehe 09 Desemba, 2015.
Napenda kuwahakikishia kwamba, kama
ilivyokuwa kwa Serikali za awamu zilizopita, Serikali ya Awamu ya Tano
itafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuhakikisha kwamba Uhuru, Amani
na Umoja na wa Taifa letu hauchezewi na mtu, kikundi au Taifa lolote.
Tutaendelea kudumisha Uhuru wetu na Mapinduzi ya Zanzibar, tunu ambazo ni msingi wa Muungano wetu na Utanzania wetu.
Tofauti na ilivyozoeleka tumeamua mwaka
huu kusherekea kumbukumbu hizi kwa kufanya kazi,. Wakati tunapata Uhuru
Taifa letu lilikuwa likiongozwa na kauli mbiu ya UHURU NA KAZI.
Kauli hii ilikuwa na lengo la kuamusha
moyo na uzalendo wa kufanya kazi miongoni mwa Watanzania kwa kutambua
kuwa uhuru wetu hautakuwa na maana kama hatutafanya kazi kwa juhudi na
maarifa ili kujenga Taifa linalojitegemea.
Watanzania katika miaka ile waliitikia
wito huo kwa kufanya kazi za kuwaongezea kipato na za kujitolea katika
kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwaletea maendeleo.
Katika miaka ya hivi karibuni moyo na
uzalendo wa kufanya kazi miongoni mwetu umepungua sana. Kwa sababu hiyo,
niliamua kutumia siku ya kumbukumbu za uhuru wetu mwaka huu
kukumbushana na kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya UHURU NA KAZI kwa
kufanya kazi hususan ya usafi wa mazingira. Madhimisho ya Uhuru mwakani
yatasherehekewa kama kawaida.
Nawapongeza viongozi wa Mikoa na Wilaya
na wa Taasisi za umma na binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali
yaliyojitokeza katika kuhakikisha kuwa zoezi la usafi wa mazingira
linafanikiwa.
Napenda kutoa wito kwa Halmashauri zote
nchini kuhakikisha zinaweka mifumo na taratibu thabiti zitakazowezesha
usafi wa miji yetu kuwa endelevu.
Viongozi wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri
waache visingizio, uwezo na mamlaka ya kuhakikisha kwamba usafi katika
miji yao unadumishwa wanao. Uwezo wa utendaji wao utapimwa pia kutokana
na hali ya usafi wa miji yao.
Naomba wananchi tushirikiane katika
kuhakikisha kuwa nyumba na mazingira ya nyumba zetu yanakuwa safi na
maji ya kunywa katika maeneo ambayo hayawekwi dawa yanachemshwa.
Aidha, wananchi wajizuie kutupa taka
ovyo na viongozi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wahakikishe
kwamba kila nyumba inakuwa na choo.
Tutashinda vita dhidi ya maradhi kama kipindupindu ikiwa sote tutazingatia kanuni za afya. Kila mtu atimize wajibu wake.
Mwalimu alisema Uhuru na Kazi na mimi nasema Hapa Kazi Tu.
December 10, 2015
Salam za Rais Magufuli kwa Wananchi katika Kuadhimisha Miaka 54 ya Uhuru
Tags
About Unknown
Templatesyard is a blogger resources site is a provider of high quality blogger template with premium looking layout and robust design. The main mission of templatesyard is to provide the best quality blogger templates.
Related Posts:
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment