HALI ya afya ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Leticia Nyerere si nzuri.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, Leticia amelazwa katika Hospitali ya Doctors Community iliyopo Maryland nchini Marekani.
Chanzo
hicho kimeeleza kuwa mwanasiasa huyo amelazwa katika Chumba cha
Wagonjwa Mahututi (ICU), ingawa haijafahamika anasumbuliwa na tatizo
gani.
Tangu
juzi usiku, kumekuwapo na taarifa nyingi kupitia mitandao mbalimbali ya
kijamii zinazodai kuwa Leticia amefariki dunia, jambo ambalo si kweli.
Habari za uhakika ambazo zimepatikana kutoka kwa mmoja wa wanafamilia ya Nyerere ni kwamba Leticia yupo hai ingawa anaumwa.
“Hali
ya Leticia si nzuri yuko ICU nchini Marekani, kwa muda mrefu sasa
amekuwa akiumwa. Tumejaribu kuwasiliana na mmoja wa watoto wake kule
Marekani, ametwambia hali si ya kuridhisha kabisa.
“…tunamwombea
Mungu ampe nguvu ili arudi katika hali ya kawaida. Tumeshangazwa na
uvumi wa taarifa hizi kwenye mitandao ya kijamii kuwa amefariki dunia,
jamani hebu tuwe na subiri ya kuwaombea wenzetu wanapokuwa kwenye
matatizo na si kukimbilia kusema fulani kafa,” alisema mwanafamilia huyo.
Leticia
aliolewa kisha kutengana na mtoto wa Hayati Baba wa Taifa, Madaraka
Nyerere mwaka 1996, ambapo walifanikiwa kupata watoto watatu.
Jana
Msemaji wa Familia ya Mageni Msobi, John Shibuda, alikiri kuugua kwa
mbunge huyo wa zamani, huku akisita kueleza ugonjwa unaomsumbua.
“Ni
kweli Leticia anaumwa na amelazwa Marekani na hali yake si nzuri, kwa
sasa tunawasiliana na madaktari pamoja na wanafamilia walioko huko kwa
ukaribu zaidi.
“Siwezi
kusema ugonjwa kwa sasa kwani suala hilo ni siri kati ya mgonjwa na
daktari wake ila sisi kama familia tutaeleza kwa kina wakati
utakapofika,” alisema Shibuda.
Julai 27 mwaka huu, Leticia alitangaza kuihama Chadema na kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akitangaza
uamuzi wake, Leticia alisema aliamua kuihama CCM baada ya kutoridhishwa
na baadhi ya mambo wakati huo. Hata hivyo alikiri kuwa alikurupuka
katika kufikia uamuzi huo.
“Moyo
wangu umekuwa ukisononeka kutokana na kukaa Chadema na kuacha kukaa
katika chama kilichonilea na kunisomesha nje ya nchi, sasa nasema narudi
nyumbani kukitumikia chama changu,” alisema.
No comments:
Post a Comment