December 30, 2015

Jinsi Majambazi Walivyotoa Uhai wa Meneja wa Zantel Kwa Kumpiga Risasi.....

Meneja wa operesheni wa kampuni ya huduma za simu za mkononi ya Zantel, Gabriel Rafael ameuawa kwa kupigwa risasi na majambazi.

Tukio hilo limetokea jana saa 4:45 asubuhi eneo la ofisi za kampuni ya Nabaki Afrika, iliyopo Mwenge, mita chache karibu na kampuni ya Coca-Cola.

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alisema haikujulikana mapema meneja huyo alikuwa akitokea wapi na gari lake aina ya Toyota Double Cabin.

Alisema baada ya kupata taarifa za mtu kuuawa kwa kupigwa risasi, polisi walifika eneo la tukio na kubaini kuwa meneja huyo alikuwa amepigwa risasi kwenye kwapa la mkono wa kulia.

Kamanda Wambura alisema ndani ya gari la mfanyakazi huyo walikuta simu, laptop na fedha taslimu Sh1 milioni.

“Mwili wake umepeleka kuhifadhiwa Hospitali ya Mwananyamala na polisi wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo pamoja na kuwasaka waliofanya mauaji hayo,” alisema Wambura.

Taarifa za mauaji ya meneja huyo zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii jana mchana zikieleza kuwa, alikuwa akitokea benki kuchukua fedha.

Katika hatua nyingine, Wambura alitoa rai kwa wakazi wote kutumia njia za kiteknolojia kuchukua na kuhifadhi fedha badala ya kutembea nazo mfukoni.   

No comments:

Post a Comment