October 4, 2015

Magufuli Ahofia Kuibiwa Kura Zake.....Awataka Wananchi Wasikubali Kudanganywa na Watu Wanaozunguka Kununua Kadi Za Kupigia Kura


Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli , amewastukia watu aliowaita mafisadi wanaozunguka mitaani na kuwalaghai wananchi ili wawauzie shahada zao za kupigia kura.

Akiwahutubia wananchi hao katika mkutano wake wa kampeni kwenye mji wa Kiomboi Jimbo la Iramba Magharibi, mkoani Singida akiwa katika siku yake ya mwisho mkoani hapa, alisema mafisadi hao wakifanikiwa kununua kadi hizo hawatashindwa kuwauza wenyewe iwapo watachaguliwa kuingia Ikulu.

Aliwatahadharisha wananchi wasikubali ulaghai kwa kuwa kufanya hivyo ni kuuza haki yao ya msingi ya kumchagua kiongozi wanayemtaka.Pia  aliwataka  mawakala  wake  wasikubali  kulaghaiwa  ili  wabadili  matokeo.

“Tuna taarifa kwamba wameanza kuweka mipango ya kununua kadi za kupigia kura, msikubali ulaghai huo maana watu hao wakichaguliwa ni hatari kwa nchi, kama watanunua kadi zenu watashindwaje kuwauza nyinyi wakiingia Ikulu?” Alihoji.

Akiwa katika jimbo la Iramba Mashariki, Dk. Magufuli alimrushia kijembe aliyekuwa Mbunge wa Iramba Mashariki kwa tiketi ya chama hicho, kuwa alichelewesha maendeleo ya jimbo hilo.

Huku akimnadi mgombea wa jimbo hilo ambalo kwa sasa linaitwa Mkalama, Allan Kiula, alisema mbunge huyo aliliongoza jimbo hilo kuanzia mwaka 1995 hadi 2010 alipoangushwa kwenye kura za maoni na sasa anagombea Jimbo la Singida Mjini kwa tiketi ya Chadema.

Akizungumza bila kumtaja jina, Dk. Magufuli alisema mbunge huyo amekaa muda mrefu lakini hakuna lolote alilowachia wananchi kwani alikuwa mpiga porojo.

“Mlikosea kuchagua mbunge hapa Iramba, mbunge wenu alikaaa muda mrefu lakini amewachelewesha, yeye alikuwa mtu wa porojo tu na ndiyo maana hivi sasa ameamua kuwakimbia na kwenda kugombea jimbo lingine kwasababu anajua angeanguka huku,” alisema Dk. Magufuli na kuongeza.

“Hivi niwaulize ukiwa na paka nyumbani kwako akakimbilia porini si anabaki kuwa paka tu, sasa msifanye makosa nichagulieni Allan maana namjua kwa uchapakazi wake,” alisema.

Dk. Magufuli aliahidi kujenga nyumba za watumishi kwa ajili ya wilaya mpya ya Mkalama ili wafanyakazi wote wanaoajiriwa waishi karibu na makazi ya wananchi.

Alisema akiwa rais ataagiza kujengwa kwa nyumba za walimu ili iwe motisha kwa walimu wanaoajiriwa kufanyakazi katika Wilaya hiyo ya Mkalama.

Mgombea huyo aliwaomba wananchi wa vyama vyote vya siasa kumpa kura akiahidi kuwa atakapochaguliwa atakuwa rais wa Watanzania wote bila kubagua vyama vyao.

“Chadema mnasema people’s power, sasa hiyo power msikae nayo bure nipeni mimi Magufuli hiyo power niingie Ikulu nikawafunge mafisadi kwa makufuli yangu,” alisema Dk. Magufuli na kuamsha shangwe kwa wananchi waliokuwa wakimsikiliza.

No comments:

Post a Comment