October 6, 2015

Lowassa: Sina Rafiki CCM......Nimepanda basi la Chadema na Rafiki yangu Yeyote Anatakiwa Kupanda Basi hilo.


Mgombea urais aliyesimamishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chadema, Edward Lowassa, amesema hana rafiki yeyote aliyebaki CCM kwani marafiki zake wote wapo Ukawa.

Aidha, amewataka wananchi wa Jimbo la Monduli kutomchagua mgombea ubunge aliyesimamishwa na CCM, Namelok Sokoine na badala yake wamchague mgombea wa Chadema, Julius Karangaraiza.

Kauli hiyo aliitoa jana wilayani Monduli, kata ya Laksale, mkoani Arusha.

"Mimi nasema hivi Mbunge anayefaa Monduli ni Karangaraiza na si Namelok...namuamini na anaweza kuendeleza yale yote niliyoyaacha.”

"Ni kweli Namelok nilimshauri agombee ubunge kupitia CCM katika Jimbo la Monduli na mambo yalivyobadilika nilipohamia Ukawa nikamshauri tena ajitoe CCM lakini akakataa...," alisema Lowassa ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo aliyemaliza muda wake na kuongeza:

"Kama CCM hawatutaki watu wa Monduli kwa nini yeye aendelee kubaki CCM?. Mimi nimepanda basi la Chadema na rafiki yangu yeyote anatakiwa kupanda basi hilo.”

Awali, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, alisema Lowassa habebi mtu yeyote katika jimbo hilo zaidi ya mgombea wa ubunge wa Chadema, Karangaraiza.

"Lowassa hana mtu CCM, ndugu na marafiki zake wote wapo Ukawa, hivyo yeyote anayesema Lowassa ni rafiki yake halafu bado yupo CCM si mtu wa Lowassa," alisema Sumaye.

Alivyopokelewa
Mamia ya watu walifurika kwenye uwanja wa polisi uliopo mjini Monduli kwa ajili ya kumshuhudia mgombea huyo urais wa Ukawa kupitia Chadema, Lowassa.

Baadhi ya wananchi hao wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Monduli, Reuben Ole Kunai, walirudisha kadi za CCM na kupewa za Chadema.

Hali hiyo ilitokea baada ya Lowassa kuwasili kwenye viwanja hivyo kwa ajili ya  kuomba kura na kumnadi mgombea wa Ubunge, Karangaraiza kwa wananchi.

Kabla ya kuanza kuzungumza, Lowassa alifanyiwa mambo ya kimila na wazee wa mila wa kabila la Kimasai.

Baada ya tukio hilo, Lowassa aliwaomba  wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo wa kampeni kupigia kura kwenye nafasi ya uraia na wagombea wa Ukawa katika nafasi za ubunge na udiwani.

"Chagueni Rais wa Ukawa, Mbunge wa Ukawa na madiwani wa Ukawa...na kama CCM watawapa pesa ili muwachague nyinyi kuleni lakini msiwape kura," alisema.

"Najua watachukia sana, lakini siwezi kumsaidia mgombea wa CCM wakati mimi nipo Chadema, kama mtu amechelewa basi na hakupanda sina jinsi ya kumsaidia," alisema.

Aidha, aliwataka wananchi wa Monduli kushirikiana katika kipindi hiki kwani kuna maisha baada ya uchaguzi.

Akizungumza mara baada ya kurudisha kadi hiyo, Ole-Kunay aliwataka wananchi wa Monduli washirikiane kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment