October 15, 2015

Lowassa: Mliobaki CCM Nifuateni Chadema.


Mgombea wa urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amewataka viongozi na makada wengine waliobaki ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoroka na kujiunga na Chadema kwani hivi sasa ni wakati wa mabadiliko.

Lowassa alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa Soko jipya wilayani Biharamulo, Mkoa wa Kagera.

Lowassa alisema huu ni wakati wa mabadiliko, hivyo aliwaomba viongozi wengine ambao bado wamo ndani ya CCM kujiunga na Chadema.

“Kama viongozi wengine bado wapo CCM wanataka kuja Chadema waje ili tuungane katika safari hii ya mabadiliko,” alisema.

Aidha, alimpongeza Katibu Mkuu mstaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi Juma Mwapachu, kwa uamuzi wake wa kujiondoa CCM na kujiunga na wana-mabadiliko.

Akizungumzia walimu, Lowassa alisema akiingia madarakani hatataka kusikia mishahara na posho za walimu zinachelewesha.

Lowassa alisema akiingia madarakani atahakikisha walimu wanalipwa vizuri ili wawape wanafunzi elimu bora.

“Sitaki kusikia kuna mizengwe mizengwe ya walimu kucheleweshewa mishahara au posho,” alisema Lowassa.

Aidha, mgombea huyo alisema akiingia madarakani atahakikisha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linaanzisha vyuo vya Elimu ya Ufundi Stadi (Veta) ili vijana wanapomaliza mafunzo wanatoka na utaalamu.

“Nataka ndani ya JKT kuwe na vyuo vya ufundi vya kufundisha watu kutengeneza pikipiki, baiskeli hata na magari. Nina imani kwa miaka mitano tutapata wataalamu wazuri,” alisema.

Aidha, alimpongeza Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, kwa kuijenga Chadema, akisema imekuwa imara na yenye nguvu.

Kabla ya kuwahutubia wananchi, Lowassa aliwaomba watulie kwa dakika kadhaa kwa ajili ya kumkumbuka Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ambaye jana Watanzania waliadhimisha kumbukumbu ya miaka 16 ya kifo chake.

No comments:

Post a Comment