Ndivyo unavyoweza kusema baada mastaa wapendanao, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ kujikuta wakipishana kauli kutokana na mvutano wa kibiashara unaohusu Sherehe ya Arobaini ya mtoto wao mchanga, Latiffah Nasibu ‘Tiffah’ ambaye amedhaminiwa Sh. Mil. 40 na makampuni mbalimbali yanayojishughulisha na bidhaa za watoto, Ijumaa Wikienda lina ‘full’ stori.
Mtoto wa Diamond na Zari, Latiffah Nasibu ‘Tiffah'.
TUJIUNGE NA CHANZO
Kwa mujibu wa chanzo, mvutano wa wawili hao umeanzia katika suala la kujadili eneo la kufanyia sherehe hiyo inayotarajiwa kufanyika Septemba 20, mwaka huu ambapo Diamond anataka sherehe ifanyikie katika ukumbi mkubwa kama yalivyopendekeza makampuni hayo yanayogombea ubalozi na kudhamini tukio hilo lakini Zari anataka ifanyike nyumbani.
“Diamond amefuata biashara zaidi. Makampuni yanayodhamini shughuli hiyo yamemwambia ili azma yao ya kutangaza bidhaa zao itimie, inabidi wafanyie kwenye ukumbi mkubwa ili watu wengi waweze kuhudhuria katika tukio hilo la kihistoria na wao waweze kutangaza bidhaa zao.
ZARI ASIMAMIA MILA ZA KWAO
“Zari ametaka shughuli hiyo ifanyikie nyumbani kwani mila za kwao Uganda zinataka shughuli hiyo ya kumtoa mtoto ifanyikie nyumbani na si katika ukumbi. Sasa Diamond alisukumwa na sababu za kibiashara na kujaribu kumshawishi mama la mama (Zari) naye akubali kupindisha mila za kwao ndipo walipotofautiana,” kilivujisha ubuyu chanzo chetu.
DIAMOND ADATA
Chanzo hicho kilizidi kujipambanua kuwa, kufuatia kupishana huko, Diamond alichanganyikiwa maana tayari makampuni yameshaanguka saini na yanahitaji shughuli hiyo ifanyike kwenye ukumbi ili malengo yao yatimie waweze kuwafikia watu wengi.
“Diamond amechanganyikiwa, anakosa jibu la moja kwa moja kwa makampuni japo anaweza kuzungumza nao wakamuelewa lakini kama akifanyia kwenye ukumbi atawafurahisha zaidi wadhamini,” kilisema chanzo hicho.
MAJIRANI WAMSHAURI
Ndugu wa karibu na Diamond ambaye hakupenda jina lake lichorwe gazetini alipenyeza habari kuwa, kuna majirani walishauri kama ikiwezekana shughuli hiyo waifanyie nyumbani siku moja kabla ya Septemba 20 ili ikifika Septemba 20, watafute ukumbi maalum kwa ajili ya sherehe hiyo.
“Yeah! Kuna majirani hapa wameshauri tufanye sherehe hii hapa nyumbani kabla ya tarehe 20 ila siku hiyo kuwe na ulinzi maalum watu wasiweze kuvujisha picha ambazo zinatakiwa kuonekana rasmi Septemba 20 kwa idhini ya wadhamini, Diamond na Zari wanaufanyia kazi pia ushauri huo,” alisema ndugu huyo wa Diamond.
DIAMOND ANASEMAJE?
Alipotafutwa Diamond kuhusiana na mvutano huo, alikiri kutokea na kuweka bayana kuwa suala hilo limemchanganya sana.“Daah hili suala limenichanganya sana. Kuna watu wanashauri tufanye ukumbini, wengine wanakataa, wengine wanataka tufanye nyumbani na ukumbini.
“Kuhusu ukumbini dini inakataa, sherehe hii inapaswa kufanyikia nyumbani nitajua cha kufanya siku zikikaribia nitakujuza utaratibu kamili,” alisema.
Chanzo-GPL
Chanzo-GPL
No comments:
Post a Comment