September 22, 2014

ONGEZA MVUTO WAKO KWA SHANGA ZA KIAFRIKA !FAHAMU MENGI HAPA


Na Kelvin Matandiko-Mwananchi
Kwa miaka mingi, jamii za Kiafrika zilikuwa na mazoea yaliyojengewa msingi katika mila na utamaduni kupitia ulimbwende wa kunogesha vazi kwa ladha ya shanga.
 
Waafrika walikuwa wakitumia vazi hilo kama sehemu ya kuongeza hadhi zao au kuashiria ufahari hususani katika familia za machifu.
 
Kadri siku zinavyoenda mambo yamekuwa yakibadilika. Kwani mtindo huo kwa sasa umekuwa ukitumiwa hata na mastaa mbalimbali ndani na nje ya bara hili kupamba mavazi yao.
 
Kwa kawaida shanga hizi hubuniwa katika rangi na maumbo mbalimbali. Kwa mantiki hiyo, huweza kuendana na kila mvaaji.
 
Kama ilivyo kwa mavazi mengine, unapoamua kutoka na pambo hili, yapo mambo ya muhimu unayopaswa kuzingatia.
 
Mambo hayo ni pamoja na mazingira, mpangilio na aina ya shanga zenyewe.
 
Licha ya ukweli kuwa shanga hizi zinaweza kuvaliwa na wanawake na wanaume, sifa nyingine ya ziada ni kwamba, zinaweza kuvaliwa na watu wa rika lolote.
  
Kuhusu mpangilio, shanga hizo mara nyingi hupendeza kijana anayevaa kwa kuchanganya ladha ya vazi husika.
  
 Kwa mfano shanga nyeusi hupendeza inapovaliwa kwenye shati au tisheti nyeupe.
 
Katika upande wa mazingira ya uvaaji, vijana wengi wamekuwa wakionekana kupendeza kwa tisheti nyeusi au nyeupe pale wanapokuwa sehemu za starehe.
 
Huvaliwa mara nyingi na kundi la wasanii wa muziki, wacheza filamu, watu maarufu au wa kawaida kabisa.
Imeandaliwa na Kelvin Matandiko

No comments:

Post a Comment