Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana
na kufanya mazungumzo na viongozi wanne Ikulu Jijini Dar es salaam
ambapo pamoja na kutakiana heri ya Mwaka Mpya, wamezungumzia mambo
mbalimbali kuhusu mustakabali wa Serikali ya awamu ya Tano ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Akizungumzia
yaliyojiri katika Mazungumzo hayo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG) Profesa Mussa Juma Assad amesema wamezungumzia kupunguza gharama za matumizi ya kuendesha serikali na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Profesa
Assad amebainisha kuwa Rais Magufuli ametaka Ofisi ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ihakikishe Tanzania inaongeza
ukusanyaji wa mapato kutoka asilimia 14 ya pato la Taifa (GDP) kwa
mujibu wa hesabu zilizofanyika mwaka juzi.
"Hadi
Mwaka juzi Tanzania ilikua inakusanya mapato kwa kiwango cha asilimia
14 ya pato la Taifa ikilinganishwa na Kenya ambayo ilikua ikikusanya
asilimia 19 ya pato Taifa, na hakuna sababu za Msingi za kwa nini
Tanzania iwe nyuma katika ukusanyaji wa mapato hayo" aliongeza Profesa Assad.
Rais Magufuli pia amekutana na Mkurugenzi wa Mashitaka hapa Nchini (DPP) Mheshimiwa Biswalo Eutropius Mganga ambaye amesema mazungumzo yao yalijikita katika suala la kupeana mikakati
ya namna ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka inavyopaswa kufanya kazi ili
kuendana na kauli mbiu ya serikali ya awamu ya tano isemayo "Hapa Kazi
Tu"
Aidha
Mganga ameongeza kuwa wamezungumzia umuhimu wa kuwahimiza watanzania
kufuata sheria, na kwamba ofisi yake itatekeleza wajibu wake bila
kumuonea mtu.
Kiongozi
Mwingine aliyekutana na Rais Magufuli ni Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh
Abubakar Zuber Ally ambaye pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa
juhudi kubwa alizoanza nazo katika uongozi wake, amesema waislamu wote nchini wanamuunga mkono na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ili aendelee na juhudi hizo.
"Na
pia kwa niaba ya Waislamu tunataka kumueleza kwamba kazi anayoifanya ni
kazi ambayo tunairidhia na tunamuomba aendelee kuifanya wala asiogope,
na kauli yake ya Hapa Kazi Tu iendelee, kwa sababu inaonesha kwamba sasa
nchi yetu itakaa mahali pazuri" Alibainisha Mufti Mkuu
Kiongozi
Mwingine aliyekutana na Rais Magufuli ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Alhaji Abdallah Majura Bulembo
ambaye amempongeza Mheshimiwa Rais kwa kasi nzuri aliyoanza nayo katika
kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015- 2020 na kutaka kasi
hiyo iendelee.
Amesema Jumuiya ya Wazazi inaunga mkono kazi kubwa inayofanywa na Rais Magufuli na kwamba Mheshimiwa Rais amemuhakikishia kuwa ataendelea kufanya kazi hizo zaidi katika kutekeleza Ilani ya CCM.
"Tunafurahi
kwamba yapo mambo mengi ambayo Rais Magufuli ameanza kuyatekeleza kwa
haraka, mojawapo likiwa ni kufutwa kwa ada za shule, na hivi sasa
wanafunzi watakwenda shule pasipo kutozwa ada" alisisitiza Alhaji Bulembo
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
04 Januari, 2016
No comments:
Post a Comment