December 3, 2015

Watu Wawili Wafikishwa Mahakamani Kwa Kutaka Kumuua Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva


WATU wawili wakiwemo Mwanasheria na Mwalimu, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya kula njama za kumuua Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva na familia yake.

Washitakiwa hao, Mwalimu Samwel Gikaro (30) na Mwanasheria Angela Mbonde (32) walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Thomas Simba.

Wakili wa Serikali, Hellen Moshi alidai kati ya Oktoba 23 na Novemba 16, mwaka huu katika maeneo tofauti Dar es Salaam na maeneo mengine nchini, washitakiwa na wengine ambao hawajafika mahakamani, walikula njama za kumuua Jaji Lubuva na familia yake.

Washitakiwa walikana mashitaka na upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo unaendelea na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa. 
 
Wakili wa upande wa utetezi, Moses Kaluwa ambaye alifika mahakamani hapo kwa niaba ya Wakili Peter Kibatala, aliiomba mahakama itoe dhamana kwa washitakiwa kwa kuwa mashitaka yanayowakabili yana dhamana.

Wakili Moshi alidai Jamhuri inatambua mashitaka hayo yana dhamana kisheria, lakini inaomba dhamana izuiliwe kwa muda hadi watakapoona inafaa kwa sababu ya asili ya kosa, washitakiwa hawawezi kuwa nje wakati upelelezi unaendelea.

Hata hivyo, Wakili Kaluwa alidai sababu zilizotolewa na upande wa jamhuri hazina msingi kisheria, suala la msingi ni mashitaka yanayowakabili kuwa na dhamana na washitakiwa wapo tayari kutimiza masharti yatakayotolewa na mahakama.

Hakimu Simba alisema pamoja na mashitaka hayo kuwa na dhamana kisheria, kutokana na kosa pamoja na hatua ya upelelezi, mahakama imekubali hoja za upande wa jamhuri hivyo washitakiwa watakuwa rumande. Kesi itatajwa tena Desemba 15, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment