December 3, 2015

CHADEMA Wasema Magufuli Anatekeleza Sera za Wapinzani


Wakati Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, John Magufuli akionekana kuteka hisia za Watanzania wengi, Chama  cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),  kimesema hakishtushwi kwani amekuwa akitumia  hoja, mikakati na Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho.

Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu, amesema kuwa wakati wa kampeni Chadema ilieleza jinsi ya kupambana na  ufisadi, kuwa na utaratibu bora wa utendaji kazi, uadilifu na uzembe wa watumishi wa umma, mambo ambayo sasa yanafanywa na Dk Magufuli.

Hata hivyo, alisema kwa kuwa anachofanya hakikuwamo katika mipango ya Chama cha Mapinduzi (CCM), anaamini atakumbana na changamoto siku zijazo.

 “Akiomba ushauri tutatoa kwa maana namna gani atekeleze, lakini ni mapema mno kusema kama ana dhamira ya kuyafanya. Pengine anayafanya kwa ajili ya kujitafutia umaarufu wa harakaharaka,” alisema Mwalimu.

Mikakati ya Dk Magufuli
Tangu Novemba 5 mpaka sasa, Dk Magufuli ametangaza mikakati kadhaa ya kubana matumizi ya Serikali, ili kuimarisha huduma za jamii, sambamba na kufichua na kuminya mianya ya rushwa na ufisadi.

Miongoni mwa mambo aliyoyafanya ni kusitisha safari za nje, kupiga marufuku michango ya aina yoyote kwa wanafunzi wa darasa la kwanza hadi kidato cha nne, kufuta sherehe za Uhuru zilizotajwa kufanyika Desemba 9 na kuagiza fedha za sherehe hizo zitumike kujenga barabara pamoja na kuibua madudu ya ukwepaji wa kodi la rushwa katika Mamlaka ya Bandari (TPA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mwalimu alisema mambo hayo ni kati ya mengi yaliyokuwa yakipigiwa kelele na Chadema pamoja na vyama vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kabla na wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25.

“Mambo haya (yanayotekelezwa na Dk Magufuli) tulikuwa tumeyapeleka mbele ya Watanzania ili watuamini na tuwafanyie. Wananchi wanajua nini kilichotokea na si ajabu kuona wao (Serikali iliyopo madarakani) wanachukua ya kwetu na kuyafanyia kazi, maana Watanzania ndiyo walioyachagua na ndiyo waliyokuwa wakiyataka,” alisema.

Huku akitolea mfano hoja za Chadema za ujenzi wa Chuo Kikuu Dodoma (Udom) na kuandikwa kwa Katiba Mpya zilivyotekelezwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Mwalimu alisema: “Uungwana ni vitendo (Dk Magufuli) atakapokuwa anayafanya si vibaya akasema jamani haya yalikuwa si ya kwangu bali nimeyakopa kutoka kwa wenzangu.”

Alisema si vibaya kwa kiongozi au chama kuiga mambo mazuri ya chama kingine na kusisitiza kuwa lengo la upinzani ni kuona mambo ya msingi yanafanyika ili nchi iwe na maendeleo.

“Suala atafanikiwa kwa kiwango gani hilo ni suala jingine, kama  anayafanya kwa utashi au kwa kuwahadaa Watanzania hilo ni suala jingine.

Mwishowe kama si lako linakuwa na changamoto katika kulitekeleza,” alieleza.

Alisema wapinzani hawawezi kuishiwa hoja za kuikosoa Serikali ambazo nyingi zinalalamikiwa na wananchi, “Mambo yetu mengi wameyachukua ila swali linakuja je, wanaweza kuyatekeleza? Chadema ni chama chenye ubunifu wa hali ya juu katika kutafuta suluhu ya kero za wananchi.”

Alisema chama hicho sambamba na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),  wataendelea kuumiza vichwa ili kutafuta jinsi ya kuzitatua kero zinazowakabili wananchi.

“Tunachokitaka kukiona ni Watanzania wakipata haki zao na maendeleo, waishi  katika nchi yenye demokrasia, utawala bora na misingi mizuri ya sheria,” alisema Mwalimu.

Mpekuzi blog

No comments:

Post a Comment