October 15, 2015

Rais Kikwete Awaonya Wanaopanga Kulinda Kura Vituoni


Rais Jakaya Kikwete amesema watu wanaopanga kubaki katika vituo vya kupigia kura baada ya kumaliza zoezi hilo kwa lengo la kulinda kura kunaashiria uvunjaji amani, hivyo serikali imejipanga kupambana na hali hiyo siku ya uchaguzi.

Rais amesisitiza kwamba wanaopaswa kulinda kura ni mawakala pekee na si wafuasi wa mgombea ama vyama.

Akizungumza jana katika sherehe za Kilele cha Mwenge wa Uhuru zilizofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, kiongozi huyo anayemalizia muda wake madarakani alisema viongozi wanaowaagiza wafuasi wao kulinda kura wana nia mbaya dhidi ya amani ya nchi.

“Mnatakiwa muondoke kwenye vituo baada ya kupiga kura….kura utazilindaje? Mawakala ndio pekee wanaoweza kulinda. Mkikaidi hilo, hatutawavulimia. Serikali imejipanga kupambana na wale wote watakaokaidi agizo la Tume ya Uchaguzi (NEC),” alisisitiza Rais Jakaya Kikwete.

Katika shehere hizo za mwenge zilizoendana sambamba na maadhimisho ya siku ya kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Rais Kikwete aliwataka Watanzania kuchagua watu waadilifu ambao wana dhamira ya kupambana na rushwa kwa vitendo.

“Tumchague mtu ambaye hana ukabila, udini na ubaguzi wa rangi…tumchague kiongozi atakayetetea maslahi ya makabila yote 126,”alisema rais huku akimnukuu Mwalimu Nyerere aliyefariki miaka 16 iliyopita.

Sherehe hiyo ilihudhuriwa pia na Spika wa Bunge anayemaliza muda wake, Anne Makinda, wakuu wa mikoa na viongozi wengine wa ngazi tofauti serikalini na kupambwa na nyimbo za makabila na wanafunzi wa shule mbalimbali mjini Dodoma.

No comments:

Post a Comment