Ikiwa zimebaki siku 23 kufikia siku ya kupiga kura nchini, mapya yameibuliwa na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, akidai kuwa zipo njama chafu za kumdhuru na kutengeneza ushahidi wa video na picha mnato na kuzisambaza.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mbatia alidai kuwa njama hizo alizozigundua zilipangwa katika mikakati tofauti na kuhakikisha zinafanikiwa.
Alitaja mbinu ya kwanza iliyopangwa kutumika kuwa ni kumteka akiwa anaelekea nyumbani kwake au mahali popote.
Mbinu ya pili alidai kuwa ni kuwapandikiza na kuwavisha vijana sare za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambao wangemvamia mahali popote, wamteke na kumjehuri ili ionekane kuwa ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kuna mgogoro.
Ya tatu kwa mujibu wa Mbatia, ni kuwakusanya wajumbe wa chama chake na wanachama kwa pamoja ili waende kumfukuza kwenye Chama, kwa madai ya kutotekeleza majukumu yake ipasavyo.
Mbatia alidai kuwa mpango huo ulikuwa ukiratibiwa na Makamu wa Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi (Tanzania Bara), Leticia Mosore, kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Makamishna wa chama hicho taifa, Peter Mushenyela.
Alidai kuwa jama hizo zilipagwa Septemba 19, mwaka huu, kwa kumtumia fedha na tiketi ya ndege, Mushenyela aliyekuwa mkoani Kagera ili aje jijini Dar es Salaam kumsaidia Musore kutekeleza mpango huo.
Hata hivyo, Mbatia alidai kuwa Mushenyela alikataa kushiriki mpango huo na kuamua kwenda kutoa taarifa Jeshi la Polisi ambalo walifungua jalada namba KW/RB/9600/2015 siku hiyo hiyo.
Kwa mujibu wa Mbatia, mbali ya Mosore kutuma fedha za nauli kwa Mushenyela, pia alituma fedha kwa wajumbe kadhaa wa mikoa wa chama hicho ili kuwashawishi waingie katika mpango huo wa kumdhuru.
Alidai kuwa Mwenyekiti huyo wa Makamishna naye aliwasiliana na naye (Mbatia) ambapo walishauriana kuweka mtego.
Alidai kuwa mpango huo wa kumdhuru, uliwashirikisha Makamishna wanne wa chama hicho wanne ambao waliletwa jijini Dar es Salaam na kuhifadhiwa katika hoteli moja huku wakilipwa posho ya kujikimu Sh. 60,000 kwa siku.
"Fedha hizo zilikuwa zinalipwa na watu wa chama kingine cha siasa...(akikitaja), ambao walikuwa wakishirikiana na Musore, huku wakiendelea na mipango yao ya kunidhuru, kuvuruga chama changu, Ukawa na viongozi wake kwa ujumla," alidai Mbatia.
“Mimi baada ya kupata taarifa zile kutoka kwa Mwenyekiti wa Makamishna kwamba Makamu Mwenyekiti anapanga mikakati hiyo na anataka ashirikiane naye, nilimwelekeza namna ya kujipanga ili kubaini njama hizo," alidai.
Pia Mbatia alida kuwa Septemba 17, mwaka huu, Mosore aliitisha kikao na waandishi wa habari kinyume na Katiba ya chama na kuzungumza mambo ya chama ambayo hayakuwa na baraka za Chama.
Alidai kuwa katika kikao hicho, pamoja na mambo mengine, Mosore alimtuhumu yeye (Mbatia) kuwa amekidhoofisha na kutelekeza chama na kwamba amewekeza nguvu zaidi Ukawa na kujifanya Msemaji wa Chadema.
Hata hivyo, Mbatia alidai kuwa Kamati Kuu ya NCCR-Mageuzi iliyokutana Septemba 22, mwaka huu, iliamua kumsimamisha Mosoreuongozi bila kumpa barua kwa kuwa uchunguzi ulikuwa unaendea.
“Si kwamba Makamu Mwenyekiti tumemsimamisha tu, lakini pia anashtakiwa kwa kupanga njama za kutaka kunidhuru," alisisitiza Mbatia.
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Makamishna wa chama hicho, Mushenyera alisema pamoja na kulipwa fedha za kujikimu kila siku, pia waliahidiwa kupatiwa Sh. milioni 10 kila mmoja endapo wangesoma hadharani na kurusha moja kwa moja waraka ambao ulikuwa umeandaliwa na Mosore na watu wa chama kingine wa kuwachafua yeye Mbatia, mgombea Urais wa Chadema, Edward Lowassa na Ukawa kwa ujumla.
Hata hivyo, Mushenyela alikataa kutaja majina ya watu wa chama kingine kwa madai kwamba ni hatari kwa maisha yake kwa kuwa ni wana fedha nyingi wanaweza kumdhuru.
Hata hivyo, Mosore alipoulizwa kuhusiana na madai hayo ya Mbatia, alikanusha vikali akidai kuwa tangu alipozungumza na waandishi wa habari Septemba 17, mwaka huu na kutoa yake ya moyoni, hajawahi kushiriki ama kupanga njama zozote za kumdhuru Mbatia.
Kuhusu suala la kusimamishwa nafasi ya uongozi, Mosore alisema:
“Mimi sijui kama nimesimamishwa na kwanza ndiyo napata taarifa kutoka kwako na kama wangekuwa wamenisimamisha, wangenipa barua,” alisema Mosore.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camilius Wambura, alithibitisha kupokea ripoti ya Mbatia kuhusiana na madai yake ya kutaka kumdhuru.
No comments:
Post a Comment