October 14, 2015

Membe Amtaka Lowassa Aache Kujifananisha na Yesu.......Asema Hana Ubavu wa Kumfufua Balali


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye pia anaungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, hana uwezo wa kumfufua aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT),  marehemu Daud Balali.

Membe ambaye jana alionekana kwa mara ya kwanza katika kampeni za mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli, alisema Balali alikufa kifo cha kawaida na hataonekana tena.

Akizungumza na wakazi wa Lindi Mjini kwenye kampeni za mgombea huyo wa urais wa CCM, Membe alisema anajua vizuri namna Balali alivyougua hadi kufariki dunia, hivyo mgombea kuahidi kumleta mtu aliyekufa ni jambo la kushangaza.

Membe alisema Balali aliugua maradhi ya utumbo na kwenda kutibiwa nchini Marekani mwaka 2008 na baadaye alifariki dunia na kuzikwa kwenye makaburi ya huko huko.

“Lowassa aache kujifanya Yesu kwamba atafufua wafu,”alisema...."nimesikia hata hapa Lindi ameshafika, sasa kamwambieni yeye si Yesu na wala hana uwezo wa kumfufua Balali,” alisema Membe.

Membe alisema kama kweli  Lowassa anaamini kwamba Balali amefichwa na serikali, basi aende akamtafute alikofichwa na amlete na kumwonyesha hadharani.

Aidha, alisema Lowassa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, wamekuwa wakidai kwamba serikali haijafanya lolote tangu uhuru wakati nao walikuwa na nafasi kubwa serikalini.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Salma Kikwete, naye aliibuka jana kwenye kampeni za Dk. Magufuli kwa mara ya kwanza na kusisitiza kuwa Dk. Magufuli ndiye chaguo bora.

Alisema rais mwenye uwezo wa kuwaletea maendeleo ya kweli na ya haraka, ni Dk. Magufuli.

Kwa upande wake, mgombea ubunge Jimbo la Mtama, Nape Nnauye, alisema ingawa kuna wanaomwandama, lakini tayari yeye ndiye atakuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka mitano ijayo.

Alisema wananchi wa Lindi na Mtama wameshaamua kumpa kura zote Dk. Magufuli kwa sababu wanaami kuwa rasilimali gesi  na mafuta iliyogundulika mkoani humo itakuwa salama.

Kwa upande wake, Dk. Magufuli alisema anataka gesi iliyogunduliwa katika mikoa ya Mtwara na Lindi iwanufaishe Watanzania wote wakiwamo wa mikoa hiyo.

Alisema atahakikisha makampuni ya nje yanayokuja kuwekeza kwenye mikoa hiyo yanaajiri wakazi wa mikoa hiyo kwa nafasi mbalimbali badala ya kwenda na watu wao.

No comments:

Post a Comment