Mwanamke mmoja mtu mzima, ambaye jina lake halikufahamika mara moja amekutwa akiwa ndani ya nyumba ya mtu pasipo kueleweka namna alivyoingia, kwani milango yote ilikuwa imefungwa kwa ndani.
Tukio hilo lilijiri hivi karibuni majira saa 2 asubuhi maeneo ya Majengo, wilayani Misungwi, mkoani Mwanza na kujaza watu wengi.
Shuhuda wa tukio hilo amesema kuwa walisikia kelele za mtu akiomba msaada na walipotoka nje, walimuona mwanamke huyo akitoka ndani ya nyumba hiyo na kuanza kutimua mbio.
“Baada ya kumkimbiza na kumkamata, tulimuweka chini ya ulinzi na kumhoji, akashindwa kujieleza kwa usahihi, tukaamua kumuachia aende zake, lakini kuna baadhi ya watu hawakuridhika, wakaendelea kumhoji, ndipo akatoa hirizi na pasipoti za watu ambazo hakusema anazitumia kwa mambo gani,” kilisema chanzo hicho kilichoomba hifadhi ya jina lake.
Mama wa nyumba iliyotokea tukio hilo, aliyejitambulisha kwa jina la Mama Neema, alisema asubuhi ya siku hiyo saa 1 asubuhi aliagana na mumewe aliyeelekea kazini kabla ya kufunga milango yote kwa makomeo na kulala.
“Nimeamka saa 2 asubuhi nikamkuta huyo bibi amekaa sebuleni, nikamuuliza wewe ni nani? Unatafuta nini humu na umepitia wapi?, hakujibu kitu ndipo nikatoka nje na kuanza kupiga kelele.
“Wakati naendelea kupiga kelele nikakumbuka mwanangu nimemuacha ndani amelala, nikarudi maana nilihisi angemdhuru, wakati nafungua mlango yule bibi alitoka nduki hapohapo watu waliokuwa wamekusanyika nje walianza kumkimbiza.”
Alisema baada ya kubanwa na kushindwa kutoa maelezo ya kuridhisha juu ya picha na madawa na hirizi aliyokutwa nayo, wananchi hao waliamua kuita polisi ambao walimpeleka kituo cha Polisi Misungwi kwa mahojiano zaidi.
No comments:
Post a Comment