October 17, 2015

Filikunjombe Alivyotikisa Bunge.........Aliwahi Kukusanya Saini Kumng'oa Waziri Mkuu, Alikataa Mabilioni ya Escrow, Alitaka Mawaziri Wazembe Wachapwe Bakora

Deo Filikunjombe akiweka sahihi katika fomu ya majina ya wabunge wasiokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
***
Bunge la Jamhuri ya Muungano halitamsahau marehemu Deo Filikunjombe, kwa umahiri na ujasiri wa kujenga hoja bungeni na kuikosoa serikali ya chama chake Chama cha Mapinduzi (CCM).

Alikuwa hana hofu licha ya nyakati nyingine kuitwa mpinzani.  Japokuwa alikuwa mwanachama mwaminifu wa CCM, alijitihidi kujenga hoja ziliozokuwa na mwonekano wa kitaifa zaidi, pasipo kuegemea siasa za chama chake. Baadhi ya mambo atakayokumbukwa nayo ni pamoja na:

Shinikizo Kwa Waziri Mkuu
Ameacha historia kwa uamuzi wake wa kutia saini fomu iliyoandaliwa bungeni na kambi ya upinzani kukusanya saini za wabunge ili kwa pamoja kushinikiza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ajiuzulu kutokana na Bunge kutokuwa na imani naye.

Wabunge hasa wa kambi ya upinzani walitaka Pinda ajiuzulu, kutokana na utendaji usioridhisha na kuwataka wabunge bila kujali vyama vyao kumpa kiongozi huyu wa shughuli za serikali bungeni,  shinikizo la kuondoka.

Pinda alitakiwa kujiuzulu kutokana na ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), pamoja na taarifa za mwaka za Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma, za kila mwaka kujaa ufisadi na ulaji wa fedha za umma, bila watuhumiwa kuchukuliwa hatua.

Escrow
Filikunjombe alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesbu za Serikali (Pac).

Katika kikao cha Bunge cha Novemba mwaka jana, akiwa na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, waliwasilisha Ripoti ya PAC iliyochunguza uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Escrow, zilizokuwa zimehifadhiwa Benki Kuu (BoT).

Hivi ndivyo alivyoshauri wakati akisoma ripoti ya PAC,:...”uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali utenguliwe mara moja na ashitakiwe kwa matumizi mabaya ya ofisi yaliyosababisha upoteza mabilioni ya fedha za umma…”

Kadhalika kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alimkosoa hivi: “Waziri Mkuu alikuwa na taarifa zote kuhusiana kuchota fedha kwenye akaunti ya Escrow, kwa mujibu wa ushahidi ulioletwa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), lakini hakuchukua hatua kuzuia muamala huo.

"Waziri Mkuu alikuwa analijua jambo hili ndiyo maana katika maelezo yake bungeni alilithibitishia Bunge kuwa fedha za Escrow hazikuwa za umma…”

Februari 2012, Filikunjombe alionyesha makeke zaidi pale alipomtaka aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mustapha Mkulo, pamoja na wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe, kujiuzulu nyadhifa zao kwa kushindwa kutimiza ahadi ya Rais ya kununua mahindi kwa wakulima wa mikoani wakiwa wa jimbo lake.

Shinikizo hilo ni moja ya mambo yaliyomuondoa Waziri Mkulo kwenye wadhifa huo na nafasi yake kuchukuliwa na Dk William Mgimwa, ambaye alifariki Januari mwaka jana.

Mawaziri wavivu
Filikunjombe alikosoa bungeni kuwa Tanzania haiendelei kwa kuwa mawaziri hawafanyi kazi. Akichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, alisema wanaofanya kazi kikamilifu hawazidi 10. 
  
Aidha wakati wa michango yake, aliliomba Bunge kubadilisha kanuni ili mawaziri wasiojibu maswali kikamilifu wapigwe viboko bungeni ili wakawaonyeshe wakwe zao.

Alikerwa na mawaziri kushindwa kujibu maswali kikamilifu na badala yake kufanya mizaha na kejeli kwa wabunge wanaouliza maswali.
 
Kutokana na msimamo wake wa kuwavalia ‘njuga’ mawaziri wavivu, ambao mahala pengine waliitwa ‘mawaziri mzigo’ alijijengea heshima kubwa machoni mwa Watanzania wa kada zote na wenye itikadi tofauti za kisiasa.

Wakati Fulani alidiriki kuwaambia wabunge wenzake wa CCM kuwa wasifikiri wenzao wa upinzani ni maadui zao, bali maadui wanaoangusha chama chao, ni watendaji serikalini, ambao hawatimizi majukumu yao ya kuwatumikia wananchi.

Kutounga mkono hoja
Hakuogopa kusema ukweli, kwenye vikao vya Bunge mwaka huu, alikataa kuunga mkono hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa Bunge la Bajeti. Hakuwa mtu wa kuburuzwa.

Kutokana na msimamo wake, wakati mwingine alikuwa akizungumza `lugha moja’ na wabunge wa upinzani, kuliko wale wa chama chake, CCM.

Aliikosoa serikali kuwa siyo sikivu na imekuwa na uzembe katika utekelezaji wa mambo muhimu na haichukui hatua kwa viongozi na watendaji wabadhirifu, mafisadi na wasiotimiza wajibu wa kutumikia umma. 
  
Katika kushughulikia ufisadi, Filikunjombe hakuwa na simile na wakati wote akiwa mbunge alipiga vita uhalifu huo.
Mpekuzi blog

No comments:

Post a Comment