Katika hali ya kumsuta Kingunge aliyetangaza kuachana na CCM hivi karibuni, Makamba alisema mwanasiasa huyo amekosa hofu ya Mungu kwa kusema uongo dhidi ya chama hicho tawala.
Makamba alisema hayo jana kwenye mkutano wa kampeni za mgombea ubunge Jimbo la Tabora Mjini kwa tiketi ya CCM, Emmanuel Mwakasaka uliofanyika kwenye viwanja vya Kituo cha Mabasi cha Zamani mjini hapa.
“Kutokana na kukosa hofu ya Mungu, kada huyo amekuwa akisema uongo na kufikia hatua ya kutaka mabadiliko bila ya kutafakari kuwa yeye alishiriki kuandika vitabu vinavyoelezea sera za chama hicho,”alisema.
Alitaja vitabu hivyo kuwa ni Mwongozo wa CCM cha mwaka 1971, Mwongozo wa CCM cha mwaka 1981, Mwelekeo wa CCM katika miaka ya 1990 pamoja na Mwelekeo wa CCM katika miaka ya 2000 hadi 2010.
Katibu mkuu huyo mstaafu alisema kutokana na ushiriki wake katika kuandika vitabu hivyo, mtu mwenye busara hawezi kusema kuwa CCM haijafanya kitu katika kuwaletea maendeleo wananchi. Aidha alisema, kama hakuna mabadiliko Kingunge hawezi kukwepa lawama.
Alisema madai ya Kingunge kwamba CCM imekosa pumzi ni kauli inayostahili kupuuzwa kwani aliingia kwenye chama hicho akiwa kijana na sasa ameondoka akiwa mzee, hali inayoashiria kuwa hawezi kuendana na kasi ya mabadiliko ndani ya chama.
Makamba alisema ameshangazwa kwa kitendo cha kada huyo wa zamani wa CCM kumpigia debe mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa wakati walishirikiana kumkataa Lowassa kwenye vikao vya Halmashauri Kuu ya Taifa kwa madai kuwa ni fisadi, hastahili kuwa kiongozi wa nchi
No comments:
Post a Comment