September 13, 2015

MSIKIE HAPA MKE WA DK.SLAA ALIVYOJIBU MAPIGO YA GWAJIMA

 


MKE wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), Dk. Willibrod Slaa, Josephine Mushumbusi,
ambaye amekuwa akitupiwa tuhuma nyingi za kumponza na kumsababishia aibu mume wake amesema kuwa hajaona jambo lolote lenye maudhui ya kujibu tuhuma zinazoelekezwa dhidi yake.
Kauli hiyo ya Mushumbusi imekuja siku chache baada ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ambaye Dk. Slaa alimtaja kama mshenga wa tukio la Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kujiunga na Chadema, kudai ana ushahidi unaoonyesha kuwa mama huyo ndiye chanzo cha mume wake kuacha siasa.
Mushumbusi ambaye yuko nje ya nchi, alitoa msimamo huo katikati ya wiki hii wakati akiwasiliana na MTANZANIA Jumamosi kwa njia ya barua pepe.
Amejipambanua kwa kusema kwamba mafanikio yake yataonekana muda si mrefu hivyo kwa sasa amefunga mikono.
“You will see my fruits bro (utayaona mafanikio yangu kaka). For now my hands closed (kwa sasa nimefunga mikono yangu,” alisema Mushumbusi.

Awali gazeti hili lilimuomba kufanya naye mahojiano kwa njia ya barua pepe juu ya mambo yote ambayo yameendelea kuibuliwa dhidi yake hata hivyo alikataa na kumueleza mwandishi wa habari hizi kwamba amruhusu aendelee na maisha yake nje ya siasa.
Katika majibu hayo, Mushumbusi alisema majungu na propaganda anawaachia wahusika na kwamba pamoja na shutuma zote zinazotolewa dhidi yake bado hajaona jambo lolote lenye maudhui ya kujibu.
“Baba niruhusu niendelee na maisha ya siasa nje ya siasa. Majungu, propaganda nawaachia wahusika…sijaona issue (jambo) yoyote yenye content (maudhui) ya kujibu,” alijibu Mushumbusi.
Mushumbusi alimweleza mwandishi wa habari hii kwamba kwa sasa hana nafasi lakini zaidi maisha yanamuhitaji hivyo hawezi kupoteza muda wake kwa vitu visivyomuongezea thamani.
“Am very busy now (sina nafasi sasa). And life is demanding too (na maisha yananihitaji pia), why should I waste time with things which are not adding any value in me? Thank you. (Kwanini nipoteze muda kwa vitu ambavyo haviniongezei thamani yoyote? Asante),”
alisema Mushumbusi. Msimamo huo wa Mushumbusi umekuja zikiwa zimepita siku chache baada ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Jesephat Gwajima, kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kujibu mapigo kwa kusema Dk. Slaa ametekwa na mke wake hivyo haiwezekani kumtoa.
Katika mkutano huo, Askofu Gwajima alisema tatizo si Dk. Slaa au Lowassa bali mtu anayechochea matatizo ni Jasephine Mushumbusi ambaye amemponza mume wake kwa kumshawishi kuachana na Chadema kisa ‘u-first lady’.
Alisema kwamba, akiwa kama rafiki wa familia hiyo, alijitahidi kutafuta usuluhishi wa mgogoro uliokuwapo kati ya Dk. Slaa na mkewe lakini jambo hilo halikufanikiwa kwa sababu Mushumbusi hakutaka kubadili msimamo.
Askofu Gwajima alisema kwamba, Mushumbusi ndiye aliyemuamuru Dk. Slaa kuacha kazi yake ya ukatibu mkuu wa Chadema. Alitolea mfano sehemu ya majibu aliyoambiwa na mke wa Dk. Slaa wakati akitatua mgogoro uliokuwapo:
“Mimi nilishajiandaa kuwa first lady na nilishaandaa biashara zangu huko nje za nchi hivyo siwezi kubadili msimamo wangu,” alimnukuu.
“Mke wake Slaa ana viashiria vyote vya matendo ya kishetani. Ni dhahiri kuwa yawezekana Slaa anayofanya yote sio akili zake,banamuendesha vibaya. Sasa kwa mfano angeteuliwa kuingia Ikulu ingekuwaje nchi hii?” alihoji Gwajima.
Kabla ya hayo kujiri, wiki iliyopita gazeti hili lilizungumza na Mushumbusi kwa njia ya simu ambapo alielezea kubeza tuhuma zote zinazoelekezwa kwake na mumewe. Katika maelezo yake alisema mambo yote yasemwayo dhidi yao hayako katika fikra zao kwa sababu wanajipanga kuelekea upande mwingine wa kuwa wawekezaji.
Mushumbusi alifafanua aina ya uwekezaji aliopanga na mumewe kuufanya baada ya kupewa fedha na marafiki zao ni kujenga shule, hospitali pamoja na kuwawezesha wanawake wajasiriamali.

No comments:

Post a Comment