September 30, 2015

Mchungaji Peter Msigwa Na Wafuasi 61 Wa Chadema Watiwa Mbaroni

JESHI  la polisi kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) mkoani  Iringa jana walitumia mabomu ya machozi kuwakamata wafuasi  zaidi ya 61  wa  chama  cha  Demokrasia  na maendeleo (chadema ) akiwemo mgombea  ubunge wao  jimbo la  Iringa mjini  mchungaji Peter Msigwa   kwa tuhuma za  kumpiga mawe mkuu wa kikosi cha  kutuliza ghasia (FFU) Iringa na   wananchi  waliokuwa  wakitoka katika mkutano  wa mgombea  Urais wa chama cha mapinduzi (CCM) Dr John Magufuli.

Imeelezwa  kuwa   wafuasi hao ambao  wengi  wao ni vijana walikuwa  wamekutana katika  eneo la kambi ya  kampeni ya Chadema  iliyopo  eneo la Hoteli  ya  Sambala jirani na kambi ya kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) kwa  ajili ya kikao cha ndani toka majira ya mchana na jioni  ndipo  walipofanya  vurugu   hizo  wakati wananchi  wakitoka katika  mkutano wa kampeni za mgombea  huyo wa Urais wa CCM.

Kamanda  wa  polisi  wa  mkoa  wa Iringa Ramadhan Mungi amewaeleza  waandishi wa habari  kuwa tukio  hilo  lilitokea   jana  majira ya saa 12;30   jioni baada  ya  wafuasi hao  kufunga barabara  kuu ya  Iringa –Dodoma  na  kufanya  vurugu  hizo kwa kuwarushia mawe  wananchi  waliokuwa  wakitoka katika  mkutano wa kampeni za Dr Magufuli uwanja  wa  Samora.

Amesema  kuwa  wakati  jeshi la polisi  likiwa katika mkutano wa mgombea  huyo wa Urais wa CCM walipokea taarifa kuwa  kuna  vijana wa  boda  boda  zaidi ya 150 walikuwa  wakijikusanya  kuelekea  katika eneo hilo la Sambala Lodge  na baada ya kufuatilia ndipo  walibaini  kuwa  wanakwenda katika  kikao chao cha  ndani  na kwa kawaida  jeshi la  polisi halikatazi  watu  kufanya  vikao  vyao vya  ndani .

“Jeshi  la  polisi  halizuii  wanachama wa  chama  chochote cha siasa  kufanya vikao vya ndani kwani  ni haki yao ya  kisheria na kikatiba,lakini  baada ya  kikao chao kumalizika  vijana hao  walitoka  nje ya ukumbi  huo uliopo kando kando ya  barabara na  kuanza  kufunga  barabara  na kucheza muziki katikakati ya barabara na kuzuia watumiaji wengine wa barabara

"Baada ya   vurugu hizo nilimuagiza mkuu wa FFU  kwenda  kuwatoa watu  hao  barabarani ila  walipuuza na kuishia kumpiga mawe  na  baadae  kukimbilia kujifungia katika Lodge hiyo ya Sambala  eneo  ambalo  wamefanya kama makao makuu ya Kampeni za Chadema  “ alisema kamanda Mungi.

Amesema  wakati wa vurugu  hizo baadhi ya  vijana  waliumia kwa  kuruka ukuta  na wengine kwa  kuanguka wakati wakijaribu  kukwepa  kukamatwa na  kuwa wale  wote waliokamatwa  watafikishwa mahakamani wakati  wowote  kuanzia  sasa na  kuwa miongoni mwao  yumo mgombea  ubunge  jimbo  hilo,Mchungaji Msigwa .

Mbali ya  mchangaji  Msigwa   wengine  waliokamatwa kwa tuhuma  za  vurugu  hizo  ni pamoja na mgombea  udiwani  kata ya  Gangilonga  ambae  pia ni mkuu wa kambi hiyo Dady Igogo

Hata  hivyo, taarifa  iliyotufikia jion  hii  inaarifu  kuwa Mchungaji  Msigwa  na wafuasi  hao 61  wameachiwa kwa dhamana leo.

No comments:

Post a Comment