Katika mada yetu ya leo, tutaangalia mambo 10 ya msingi ambayo yanaweza kukusaidia kumtambua mpenzi aliyekusaliti muda mfupi uliopita. Hapa namaanisha utaweza kumtambua mpenzi aliyekusaliti ndani ya saa 24.
Tafadhali weka mawazo yako hapa ili uweze kumgundua mwenzi ambaye ni mwizi wa haki yako. Sasa hebu twende tukaone.
RATIBA YA GHAFLA
Rafiki zangu, ukishaanza kuwa na wasiwasi na mpenzi wako kwamba huenda anataka kukusaliti, jambo la kwanza kabisa unalotakiwa kukumbuka ni sehemu aliyokuambia amepitia/anakwenda kama ilikuwa katika mipango yake au amefanya safari ya kushtukiza.
Hii ni dalili ya kwanza kabla hata hamjakutana nyumbani; “Sorry baby, kuna sehemu napitia mara moja, nitachelewa kidogo kurudi nyumbani,” kauli kama hii iangalie sana.
Mwingine anaweza kupiga simu na kusema: “Mume wangu, bosi ametupa ofa ya dina wafanyakazi wote, kwa hiyo nitachelewa kurudi nyumbani, samahani sana dear.”
Kauli hizo mbili ni alama ya kwanza katika kushibisha hoja yako ya kusalitiwa kama ni kweli atakuwa amefanya hivyo. Kumbuka kwamba, si lazima kila anayesema amepata dharura amesaliti.
ANAKWEPA KUWASILIANA
Mtu huyo ambaye ameshatoa taarifa kwamba amepata dharura, utashangaa hataki kuwasiliana na wewe. Pengine ukimpigia simu, anaweza asipokee na kama akipokea anaweza kukujibu: “Nitakupigia baadaye, samahani sipo sehemu nzuri.”
Unaweza kumwandikia meseji lakini pia asijibu. Wapo wengine vichwa ngumu zaidi, ambao wao kuacha kupokea simu na kujibu meseji si vitu muhimu sana, wanazima kabisa! Ukiona dalili hii, basi ujue unasalitiwa.
UCHANGAMFU KUPITILIZA
Pamoja na mambo hayo hapo juu, lakini mwenzi huyu akirejea nyumbani, huwa mchangamfu kupitiliza. Ana maneno mengi, anaanzisha mijadala ya ghafla na kuifunga mwenyewe. Atajifanya anataka kufanya mambo mengi kwa ajili yako.
Ahadi zake zinakuwa nyingi za ghafla na nyingi zipo wazi kabisa kwamba si rahisi kuzitekeleza. Alama hii ni kati ya zile 10 zinathibitisha kwamba ndani ya saa 24 umeibiwa mali yako.
UPOLE KUPITILIZA
Kinyume cha uchangamfu ni upole, kama mwenzi wako ametoka kimapenzi na patina mwingine kwa ile hofu yake moyoni, anaweza kuwa mpole kupitiliza. Anafanya hivyo kwa lengo la kutafuta huruma.
Hana sababu ya kuwa mpole, lakini anaweza kutumia ngao hiyo, ili maswali utakayomuuliza yawe kuhusu upole na ukimya wake, usahau mambo ya kuhisi kuwa umesalitiwa. Hata hivyo, majibu yake yanaweza kuwa ya mkato sana: “Sijisikii vizuri, siku yangu haikuwa nzuri kabisa leo. Kuna mtu nimetibuana naye ofisini, amenichanganya kabisa.”
Alama hii ni moja ya sababu zitakazokufanya uendelee kumchunguza katika hatua zinazofuata ili mwisho ugundue kuwa umesalitiwa au ni wasiwasi wako tu.
UGONJWA WA GHAFLA
Katika kukwepa usumbufu wa maswali mengi, mwingine huamua kujifanya anaumwa. Atarudi akiwa mkimya kuliko kawaida, ukimwuliza atakujibu kuwa anaumwa. Kama mpenzi wake, anajua wazi kuwa hutakuwa na muda wa kuanza kuhisi usaliti badala yake utamjali na kuuliza hali yake.
Mgonjwa huyu kwa kawaida huwa haumwi magonjwa siriasi, sana sana atakuambia hajisikii vizuri, kichwa kinamgonga au moyo unaenda mbio. Ukizungumza kuhusu suala la hospitali atakataa akidai hana hali mbaya sana. Mara nyingi hupenda kukimbilia kitandani, akitaka kupumzika.
Anafanya hivyo kwa sababu anakwepa aibu ya kukutanisha uso wake na wako. Ukitaka kwenda kumnunulia dawa za maumivu atakujibu: “Nimeshameza panadol baby.” Mwenzi wa aina hii unatakiwa umtilie mashaka, maana inawezekana ametoka kufanya kitu kibaya.
MAJIBU TATA
Mpenzi ambaye ametoka kukusaliti huwa hapendi kuulizwa maswali mengi, ukimwuliza majibu yake huwa tatanishi sana. Kwa kuwa ameshasingizia kwamba anaumwa, hivyo atafika na kulala moja kwa moja.
Ukitaka kujua zaidi kuhusu kuugua kwake au dharura aliyoipata iliyosababisha achelewe kurudi nyumbani, hukosa majibu yanayoeleweka. Wakati mwingine anaweza kujisahau na kukupa jibu ambalo linapingana na maelezo yake ya awali. Ukiona hivyo ujue kuna namna.
HATAKI FARAGHA
Kwa kuwa tayari ameshatoka kwa mtu mwingine, huhofia sana kukutana na wewe faragha. Kama tulivyoona katika vipengele vilivyopita, hutengeneza mazingira ya kukufanya msikutane kimwili, hofu yake ikiwa ni kukuficha usigundue mchezo wake mchafu.
Kisingizio cha kuumwa, bila shaka ni kikubwa na kitakufanya ushindwe kuwa na mhemko wa kimahaba, lakini kurudi nyumbani akiwa amekunja ndita au mpole kupitiliza, tafsiri yake ni wewe kuogopa au kuhamisha hisia zako kutoka kwenye mapenzi na kuanza kumfikiria yeye kama yeye.
Kwa vyovyote vile, kama ni mwenzi wako wa muda mrefu, zipo alama nyingi zitakazoweza kukufanya ujue kuwa ametoka nje, kwanza ni vyema kumkazania kukutana naye faragha. Hata kama atasingizia anaumwa, ng’ang’ania kukutana naye, maana hapa ndipo penye ukweli mkubwa zaidi.
Mchunguze anavyokupokea, halafu pima uwajibikaji wake. Huwa mvivu na asiyetaka kutoa ushirikiano. Anaweza kuishia kulalamika kuwa hajisikii vizuri na kusisitiza mhairishe zoezi hilo.
Mpenzi msomaji, njia unayopita kila siku unaijua. Sehemu yenye makorongo unaifahamu, yenye matuta pia utatambua, hata yenye makorongo yenye maji yaliyosimama pia unaijua vyema, sasa ukikutana na tofauti yoyote katika barabara unayoitumia siku zote, maana yake tingatinga limepita.
ANAKWEPA KUSOGELEWA
Akifika tu nyumbani, atahakikisha hupati nafasi ya kuwa naye karibu. Hataki kabisa kusogelewa. Hapo anakimbia vitu vitatu;
Kwanza kabisa, inawezekana huko alipotoka alitumia manukato tofauti na aliyotoka nayo nyumbani asubuhi.
Pili, manukato ya sabuni mpya aliyotumia, anaogopa usiyasikie, tatu, kila mtu ana harufu yake, unapokaa na mtu kwa ukaribu hasa faragha kwa saa mbili au zaidi, kila mmoja huhama na harufu ya mwenzake.
Kwa kuwa wewe unaitambua vyema harufu ya mpenzi wako, atahofia kukusogelea maana utashtukia. Mwisho kabisa, hata kama atakuwa amekwepa yote hayo, labda hajaoga, hajatumia manukato mengine, bado utaweza kumkamata kwa harufu ya manukato, sabuni au mafuta aliyotumia mtu aliyekuwa naye.
Kukwepa kukusogelea, tafsiri yake ni kwamba hataki usikie harufu ya tofauti kutoka kwake, maana anajua alichokifanya. Jiulize, kama kila siku huwa mnapokeana kwa mabusu na kukumbatiana, kwanini safari hii anakukwepa?
ANAKIMBILIA BAFUNI
Akifanikiwa kukuzuga katika kipengele kilichopita, basi safari yake huishia bafuni. Ataenda haraka na hatataka kwenda na wewe maana kuna kitu anajaribu kukuficha. Wengi wanaamini (kuna ukweli kwa asilimia chache) baada ya kuoga wanaweza kupoteza ushahidi wa kutoka nje ya ndoa/wapenzi wao.
Utakapomruhusu aoge, kwanza atatumia sabuni ya siku zote, ambayo anaweza kuitumia kwa wingi awezavyo ili kuficha ushahidi. Atajisafisha zaidi nyeti zake ili usijue kilichotokea muda mfupi.
Akitoka bafuni lazima atakimbilia kwenye meza ya kujipambia kisha hapo atajimiminia manukato ili kuzima kabisa ushahidi ambao ungeweza kumuumbua. Jiulize, kama kila siku huwa mnaoga pamoja, kwanini amekuja ghafla na kukimbilia bafuni bila wewe?
WASIWASI MWINGI
Atakuwa mwenye wasiwasi mwingi sana, hata kama akikubali kukutana na wewe faragha, ushirikiano huwa hafifu. Mwoga kupitiliza na muda wote huwa anahisi kwamba hatakufikisha salama safari yako.
Wasiwasi wake hauishii hapo, hata kupeana mikono tu na kukutanisha macho, kutakuonesha jinsi alivyo na wasiwasi. Si kama anapenda hali hiyo, ila anazidiwa na hisia za usaliti kwa kuwa anajua alichokifanya muda mfupi uliopita.
Kama utavifuatilia vipengele hivyo kwa makini, ni rahisi sana kumkamata mwizi wako. Acha papara, chunguza taratibu, ukiona angalau kuna nusu ya hizi nili zokupa hapo juu, ujue wazi kuwa unaibiwa tu
No comments:
Post a Comment