Baadhi ya watu jana mchana ‘waligida’ pombe za bure baada ya Fuso lililokuwa limebeba masanduku ya bia kupinduka katika Barabara ya Mandela, Dar es Salaam baada ya Fuso hilo kugongwa kwa nyuma na lori na kupinduka.
Kundi hilo la vijana hao wakiwemo madereva wa bodaboda walivamia na kuchukua chupa za bia na kunywa huku wengine wakinywa mfululizo.
Tukio hilo lilidumu kwa takribani 20 kabla ya polisi kuongeza nguvu.
Vijana wengine waliingia mitaroni ambako bia ziliangukia na kuzichukua bila kujali kuwa zimepasuka, muda mfupi baadae wengine wakaanza kulewa.
Dereva wa Fuso hilo Mohamed Said alisema mzigo huo wa bia aliutoa katika Kiwanda cha Serengeti kwenda Kituo cha Polisi Mkoa wa Pwani.
“Hizi bia zilikuwa katika masanduku 500 ni mali ya Polisi Pwani, ajali hii ni uzembe unaoonekana wazi kuwa wa dereva wa lori, hata polisi wakija kupima watajua nani mwenye kosa,” alisema Said kabla ya Fuso lingine kufika na kuchukua bia hizo na kuondoka nazo.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori aliyekuwa akitokea njia ya pembeni kuingia barabara kuu bila tahadhari japo dereva wa lori amekataa kusababisha ajali hiyo.
No comments:
Post a Comment