January 19, 2015

HATARI KUBWA DAR! MATUKIO KIBAO YA UJAMBAZI BENKI


Makamanda wa OFM (katikati) wakiwa ndani ya benki.
Stori: Chande Abdallah, Mayasa Mariwata, Shani Ramadhani na Denis Mtima 
WAKATI kukiwa na dhana ya baadhi ya wafanyakazi na wateja wa mabenki nchini kuvujisha taarifa za wateja wanaotoa kiasi kikubwa cha fedha kwa majambazi ambapo mwishowe wateja hao huvamiwa na kuporwa, Oparesheni Fichua Maovu (OFM) imetinga ndani ya benki kadhaa jijini Dar na kugundua udhaifu mkubwa katika ulinzi, ushahidi huu hapa. 

Kutokana na matukio mfululizo ya wateja kuvamiwa mara baada ya kutoka kuchukua fedha ndani ya mabenki, watu kadhaa walitoa malalamiko yao kwa OFM wakitaka suala hilo lifanyiwe kazi kwa kuwa wao wanaamini kuna udhaifu mkubwa kwenye sekta ya ulinzi. 

Wakizungumza na Ijumaa Wikienda kwa masharti ya kutotaja majina yao, baadhi ya watu hao walisema wapo wafanyakazi au wateja ambao wanaweza kuingia benki na kutoa taarifa za mteja mwingine ambaye anatoa pesa nyingi kwani ulinzi ni mdogo. 

MALALAMIKO
“Unajua ukikuta mtu anaweza kuingia benki akaongea na simu akiwa kwenye foleni ni tatizo. Siku hizi hata baadhi ya mabenki, hata wale wanaotoa huduma (teller) nao wana uwezo wa kuwasiliana kwa simu huku kukiwa na wateja na wao wakiwa kwenye madirisha yao. 

“Tabia hii ndiyo chanzo cha ujambazi mkubwa unaotokea siku hizi. Mtoa huduma anaweza kumwambia jambazi nje kwa simu kwamba kuna mtu amevaa suti anatoka na mkoba mweusi una milioni kumi kwa sababu yeye si ndiye amemtolea?

“Au wateja wanaoongea na simu wakiwa kwenye foleni, ni rahisi kuvujisha taarifa kwa majambazi. Unajikuta unakwenda kuvamiwa mbele ya safari kumbe watu walikufuatilia tangu ndani ya benki,” alisema mmoja wa watu hao.
 
Mmoja wa makamanda wa OFM akiongea na simu bila kizuizi chochote kutoka kwa walinzi wa benki.
OFM YAINGIA KAZINI
Baada ya kupokea malalamiko hayo, OFM  ilijipanga na kuanza kuzungukia benki mbalimbali jijini Dar ili kupata ukweli.  


KAZI YAANZA
Januari 12, mwaka huu, saa 7:24 mchana, makamanda wa OFM walitinga ndani ya benki  moja kubwa iliyopo maeneo ya Mnazi Mmoja, Dar, mmoja akiwa na bastola kibindoni huku mwingine akiwa na simu ya mkononi ambayo aliitumia kuongea na watu kila mara bila kuchukuliwa hatua yoyote licha ya kuwepo kwa matangazo yaliyosomeka; switch off your phone (zima simu yako).


Kama hiyo haitoshi, makamanda waliokuwa na kibarua cha kuchukua picha ya kile kilichokuwa kikiendelea ndani ya benki hiyo, walishuhudia wateja wengine wakizungumza kwa simu kwa sauti za juu huku wenzao wakitoa fedha bila kuhofia usalama wao. 

SAA 7: 43 MCHANA
Bila kutambulika, kamanda mmoja wa OFM alichukua simu yake ya mkononi na kumpigia mwenzake aliyekuwa nje na kuzungumza naye kwa sekunde 33 kisha kukata na kupiga tena ambapo alitumia sekunde 17 na kuendelea kuchati na watu wengine bila kizuizi chochote.


Kamanda mwingine aliyekuwa na bastola ndani ya mfuko alijaza fomu ya kuweka fedha (deposit slip) na kwenda moja kwa moja kwa ‘teller’ kuweka fedha zake.
 
Kamanda wa OFM akiwa na bastola ndani ya benki.
Hadi saa 8:02, makamanda wanaondoka kwenye benki hiyo, hakuna mhusika hata mmoja aliyeshtukia zoezi hilo, jambo lililoonesha kuwa uvamizi ndani ya benki au kuvuja kwa taarifa za wateja wanaohudumiwa ni rahisi kuliko inavyoweza kudhaniwa. 

BENKI YA PILI
Januari 17, mwaka huu, saa 5:16 asubuhi. makamanda wa OFM walitinga ndani ya benki nyingine iliyopo maeneo ya Mwenge jijini Dar, zoezi likiwa kama lile la awali ambapo kamanda mmoja wa OFM alibeba bastola na kujitoma nayo ndani huku mwingine akiwa na simu ya mkononi. 


Saa 5:17, kamanda wa OFM akiwa na bastola inayoonekana kuchomoza nje ya mfuko wa suruali, aliingia ndani ya benki hiyo na kujaza fomu bila kumjali mlinzi aliyekuwa pembeni.
Saa 5:19, kamanda akaelekea upande wa maulizo ambapo aliomba maelekezo ya jinsi ya kufungua akaunti na kuambiwa asubiri kwa muda.


Dakika 7 baadaye, mhudumu wa maulizo alimwita kamanda na kumpa fomu yenye maelezo ya jinsi ya kufungua akaunti na kuondoka zake.

Saa 5:21 kamanda aliyekuwa na simu alimpigia mtu aliyekuwepo nje ya benki na kuongea naye kwa dakika 2 huku hali ikiwa kama ile ya benki ya awali ambapo hakukuwa na katazo lolote kutoka kwa mlinzi wa benki  hiyo.
Timu nzima ya OFM iliondoka maeneo hayo kwa mtindo wa kijasusi bila kushtukiwa jambo ambalo kwa benki iliyojizatiti kwa ulinzi, makamanda wa OFM wangeshtukiwa mapema.
Kamanda Kova akizungumza jambo.
LENGO LA OFM
Lengo la OFM kufanya ushushu kuhusu madai ya udhaifu wa ulinzi kwenye baadhi ya mabenki, si kuzisakama benki hizo bali kuwaondoa katika usingizi mzito wa ulinzi kwani ujambazi kwa sasa jijini Dar hasa kwa wateja wanaotokea benki ni jambo la kutisha. 


Tayari gazeti hili lina mlolongo wa wateja waliopigwa risasi na kufa wakiwa wanatoka ndani ya benki kuchukua fedha. Swali ni je, majambazi hao huwa wanaambiwa na nani kwamba, mteja anayetoka amebeba ‘mzigo mnono’? 

Gazeti hili linamshauri Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kusimamia suala hili kwa karibu ili kupunguza matukio ya ujambazi katika benki

No comments:

Post a Comment