Wiki jana tulikutana hapa na kujadili jinsi baadhi ya wanafunzi wa shule, kuanzia za msingi hadi vyuo wanavyojiuza katika madanguro mbalimbali yaliyotapakaa hapa nchini, hasa katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Morogoro, Dodoma na mingineyo.
Leo tunajaribu kuangalia tabia ambazo ninaamini ni za kurithi kizazi hadi kizazi cha shule, kuanzia zile za msingi hadi vyuoni. Nimejaribu kueleza mara kadhaa juu ya kuwepo kwa tabia ya wanafunzi kujihusisha kimapenzi, wake kwa waume, wakitembea na walimu wao au wanafunzi wenzao.
Na uhusiano huu huwa una pande mbili, moja ya kulazimisha na nyingine ya kuridhia wenyewe. Baadhi ya walimu na hata wanafunzi wababe, huwatisha wasichana wadogo shuleni ili waweze kushiriki nao mapenzi na mara nyingine, wanafunzi wenyewe huridhia kutembea na walimu au madenti wenzao kwa fasheni tu, kwa sababu Rose anachukuliwa na ticha Tom basi na Asha naye anamtaka Sam.
Sasa wakati hali iko hivi, kuna upande mwingine wa pili wa shilingi kuhusiana na haya mambo. Ninakumbuka wakati tupo shule, siku moja kulitokea bonge la ugomvi kati ya washkaji wawili, kisa jamaa kuchukuliwa mpenzi wake.
Ilikuwa hivi; mshkaji mmoja tulikuwa naye kidato cha tatu alikuwa na mpenzi wake wa kidato cha kwanza, wameendelea muda kama wa miezi sita, jamaa mwingine akahamia shuleni kwetu kutoka Dar es Salaam. Unajua tena, Dar asikuambie mtu bwana, kuna ujiko sana hasa kwa wanafunzi huko mikoani
Jamaa akahamia kidato cha nne. Katika tupiatupia yake macho pale yakaenda kutua kwa huyo binti. Akamsogelea na kumwaga sera zake. Zikakubaliwa.
Wakaanzisha uhusiano wa siri bila mshkaji wetu kujua, lakini mambo ya madenti si unajua, haikupita hata wiki habari zikavuja. Basi jamaa yetu akaomba ushauri, tukamwambia tumwendee mshkaji tumweleze kuwa aachane na msichana huyo kwa kuwa tayari alishakuwa wa mtu.
Tukakubaliana. Shule yetu ilikuwa mjini, tunatoka saa nane mchana, saa kumi tunarejea kwa twisheni na mazoezi ya mpira na wengine wanakuja ili mradi tu kupiga stori hadi jioni.
Hee, si ndiyo jioni bwana tumekusanyika, yule msela kutoka Dar akaonekana anaimbisha tena msichana mwingine wa kidato cha pili, mchizi wetu akamaindi!
Basi bila kumsemesha mtu, akaondoka kumfuata mshkaji pale alipokuwa, akaenda akampiga bonge la ngwara wenyewe tunaita mtama, jamaa akadondoka kama fuko la taka. Zikafuata ngumi, watu ndiyo kukimbilia kumaliza utata.
Haikuwa hiyo tu, ngumi zimeshatokea mara nyingi tu, nyingine zinapigwa mtaani lakini sababu kubwa ni kuchukuliana wapenzi mashuleni.
Wakati ule tulikuwa kama tunaona ujanja flani hivi, yaani mtu aje kukuchukulia mpenzi wako? Tulitumia muda mwingi kuwafuatilia wapenzi wetu kama wanatusaliti badala ya kuzingatia mambo ya msingi ya masomo.
Ninajua mchezo huu bado upo, hasa katika nyakati hizi za teknolojia, ambazo watu wanaweza kuchati hadi usiku wa manane wakati bado wanafunzi. Nichukua fursa hii kwa mara nyingine kuwaasa kuwa wakati ukuta.
Mnaweza kujiona mnafanya jambo la maana hivi sasa, mkadharau masomo, lakini mtakapokuja kushtuka, mmeshachelewa. Haya mambo yapo tu, tena kama ukiwa na elimu yako ya kutosha itakayokuhakikishia maisha, mbona unapeta sana?
Hali kama hii ipo pia kwa wanafunzi wa kike, nao wanasengenyana, kupigana mafumbo, kisa, mwenzake ‘katoka’ na ‘boyfriend’ wake. Acheni!
No comments:
Post a Comment