September 17, 2014

MABWENI YA SHULE YA SEKONDARI YATEKETEA KWA MOTO YADAIWA MWANAFUNZI AMEHUSIKA KUYACHOMA TAZAMA PICHA HAPA

MABWENI mawili ya Shule ya Sekondari ya Nyansicha inayomilikiwa na Kanisa la Waadventista Wasabato, Seventh-Day Adventist Church(SDA), iliyopo katika Kata na Kijiji cha Nyanshinja Kilomita 33 katika Wilaya ya Tarime mkoani Mara yameteketea kwa moto katika mazingira ya kutatanisha.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana katika eneo la tukio, zinaeleza kuwa moto huo ulizuka juzi Jumatatu Septemba 15, 2014 saa kumi na moja jioni wakati wanafunzi wa shule hiyo wakirejea shuleni baada ya kuwa katika likizo fupi.

Taarifa zinasema awali kabla ya moto huo kuzuka alitokea mwanafunzi wa kidato cha pili (hakutambulika jina mara moja) aliingia kwenye moja ya mabweni ya shule hiyo na kuanzisha vurugu hali iliyowafanya wanafunzi kutoka nje na kumuacha akiwa ndani ambapo pia imeelezwa kuwa alijifungia ndani kwa komeo la mlango wa bweni kabla ya moto kuzuka. 

Bweni likiwa linawaka moto. 
“Haieleweki moja kwa moja kuwa moto ulisababishwa nanini kwamaana shule inatumia Jenereta na umeme wa nguvu za jua (Solar system) na mda moto uliozuka palikuwa hakuna matumizi ya umeme, na huyu mwanafunzi anaonekana kuwa na mapepo kwamaana wakati moto unawake alitaka kurudi ndani baada ya kutolewa nje ndio maana watu wamepigw ana butwaa juu ya hili tukio” kilieleza chanzo cha habari.
 Wanakijiji na wanafunzi wakitazama bweni lililoungua. 
Akizungumza na FikraPevu mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo amesema “Baada ya huyu Mwanafunzi wa kiume kujifungia ndani, moto mkubwa ulizuka kwenye bweni hilo, ndipo watu wakatafuta namna ya kuomba msaada wa kuuzima moto na kuvunja mlango ili kumtoa huyo mwanafunzi ambapo zoezi lilifanikiwa”.

Amesema mara baaada ya mwanafunzi huyo kutolewa alichukuliwa na Polisi ambapo hadi wakati huu amesekwa rumande kutokana na tukio hilo.
Wanafunzi waliweza kuokoa baadhi ya mali kama zinavyoonekana.
Mwalimu wa zamu katika shule hiyo, Joseph Nduru, amesema hadi sasa thamani ya vitu vilivyoteketea haijafahamika. Pia amesema mali zilizoteketea kwa moto ni pamoja na Magodoro yanayotumiwa na wanafunzi zaidi ya (100), mali zote za wanafunzi na kwamba vitu vilivyookolewa ni baadhi ya mabegi ya wanafunzi hao.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, John Henjewele, amesema huenda mwanafunzi huyo anamapepo kutokana na historia yake na utaratibu wa kupatiwa matibabu kutka Hospitalini zinaendelea. 

Jeshi la Polisi katika Kanda Maalum ya Tarime- Rorya limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba uchunguzi bado unaendelea.

No comments:

Post a Comment