November 2, 2014

WABUNGE TISA WAJIUZULU KUMPINGA SHY-ROSE

Mgogoro ndani ya Bunge la Afrika Mashariki (Eala) umechukua sura mpya baada ya wabunge tisa, wakiwamo makamishna watano na wenyeviti wanne wa kamati za Bunge hilo, kuwasilisha barua za kujiuzulu nafasi zao hizo, ikiwa ni matokeo ya sakata linalomhusisha mbunge mwenzao kutoka Tanzania, Shy-Rose Bhanji (pichani).

Kutokana na hali hiyo, Bunge hilo ambalo lilikutana kwa wiki mbili huko Kigali, Rwanda liliahirishwa jana kwa muda usiojulikana, muda mfupi baada ya kushindwa kufanya uamuzi wa kumwadhibu Bhanji ambaye anakabiliwa na tuhuma mbalimbali za utovu wa nidhamu.

Mgogoro huo ulisababisha Eala kwa wiki mbili, kushindwa kufanya lolote lililokuwa limepangwa kwenye kalenda yake, kwani kila lilipokutana, wabunge walitoa hoja liahirishwe hadi pale suala la nidhamu dhidi ya Bhanji litakapotolewa uamuzi.

Mbunge huyo anatuhumiwa kutoa maneno yasiyokuwa na staha kwa wenzake, kuwakashifu na kuwatukana baadhi ya viongozi wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wakati wa ziara ya ujumbe wa Eala katika nchi za Jumuiya ya Ulaya (EU), Ubelgiji.

No comments:

Post a Comment